Shirika la Uwiano wa Maendeleo Vijijini (Integrated Rural Development Organization/IRDO) limefanya uzinduzi wa mpango mkakati na uhamasishaji wa rasilimali kwa miaka mitano kuanzia mwaka huu (2024-2028). Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Ileje,Mhe. Farida Mgomi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe amezindua Mpango Mkakati wa Uhamasishaji wa Rasilimali wa Shirika la Uwiano wa Maendeleo Vijijini. Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa High Class mjini Tunduma tarehe 12 Machi 2024 na kuhudhuriwa na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo na wadau mbalimbali, Mgomi amelipongeza Shirika hilo kwa uthubutu huo wa kuonesha ushirikiano mkubwa na Serikali katika utekelezaji ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi. Mhe. Mgomi ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa shirika hilo na mashirika mengine ili kukamilisha afua zote kwa jamii zilizoainishwa katika mpango mkakati huo. “Niwapongeze sana Shirika hili la IRDO kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya katika jamii yetu…kwani kupitia miradi yenu mnaikomboa jamii na mambo mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa chakula na lishe, kupinga ukatili wa kijinsia, kutoa elimu ya kupambana na virusi vya UKIMWI na kuwasaidia kupima na kuwaonesha mahali pa kweli baada ya kubainika kuwa wana Virusi vya UKIMWI…miradi ya vijana wa kike na wakiume waliobarehe kwa kuwapatia elimu mbalimbali…kwa kweli makundi yote haya yanahitaji kusaidiwa.” Amesema Mhe. Mgomi na kuongeza; “Shirika hili limetoa fursa kwa vijana hawa wa kike na kiume ili waweze kujitambua na kujitunza na kufikia ndoto zao salama…hamkuishia hapo pia, mnashughulika na kuwasaidia vijana wetu walioathirika na madawa ya kulevya kwa kuwapatia dawa kupitia Kituo chetu cha Afya cha Tunduma…hii ni kazi kubwa na mnastahili pongezi.” Awali akiwasilisha vipaumbele vya IRDO, Mkurugenzi wa Shirika hilo, Dr. Simon Chiwanga ameeleza kuwa lengo kubwa la Shirika ni kuinua maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia miradi ya kilimo endelevu, elimu ya ujasiriamali na masoko, uhakika wa chakula, uboreshaji lishe, afya ya jamii kwa maana ya kutokomeza maambukizi mapya ya VVU na afya ya uzazi. Chiwanga ametaja malengo mengine ya Shiriki kuwa ni upatikanaji wa maji safi na salama, kutokomeza ukatili wa kijinsia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuboresha mazingira. Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mhe. Farida Mgomi (kulia) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe akiangalia bidhaa zinazozalishwa na baadhi ya wanufaika wa miradi wa DREAMS, FOSENI/Uhakika wa Chakula na Uboreshaji wa lishe, na wanufika wa mradi wa MAT ambao ni waraibu wa madawa ya kulevya unaotekelezwa na na Shirika la Uwiano wa Maendeleo Vijijini – IRDO mara baada ya kuzindua Mpango Mkakati wa Uhamasishaji wa Rasilimali wa Shirika hilo kwa kipindi cha miaka mitano (2024-2028).